Na Fatma Amri
Rais wa Baraza la vyama vya soka kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati, (CECAFA) Leodger Tenga, anaonekana kuichongea timu ya Simba kwa wapinzani wao Timu ya Awasa ya Ethiopia baada ya aliyekuwa mpinzani wa kwenye uchaguzi wa baraza hilo Ashibel Georgis kuwasaidia wapinzani wa Wekundu hao wa Msimbazi.
Aliyekuwa mpinzani wa Leodger Tenga katika kinyang’anyiro cha kuwania urais wa Shirikisho la vyama vya soka katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Ashibel Georgis amelipiza kisasi kwa kuiweka kambini Timu ya Awasa ya Ethiopia kwa ajili ya kuhakikisha inaifunga Simba.
Akizungumza na Championi, mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Dar es Salaam, afisa mmoja wa ubalozi wa Tanzania nchini Ethiopia ambaye hakupenda kutajwa jina lake, alisema kuwa Ashibel ameiweka Awasa kambini na kupa kila aina ya msaada ili kuishinda Simba ikiwa ni sehemu ya kulipiza kisasi kwa Tenga baada ya kumshinda katika uchaguzi wa baraza hilo.
Vile vile afisa huyo alifafanua kuwa Simba wanakazi ya kufanya ili kushindwa ugenini kwani tajiri huyo anaendelea kusuka mipango ili kuhakikisha kwamba wawakilishi hao wa Tanzania wapati chochote watakapokuwa ugenini.
Moja ya mipango hiyo ni kuangalia kama kuna uwezekano mchezo huo ukafanyika katika Uwanja wa Awasa ambao historia inaonesha kwamba hakuna timu kutoka nje iliyoshinda katika dimba.
Ili kuonesha hasira zake za kukosa urais wa Cecafa, Ashibel amejitolea kutoa kila aina ya msaada ambao unatakiwa ili kuipa nguvu timu hiyo jambo ambalo litaiwezesha kujiweka vyema kabla ya kukutana na Simba.
Uwanja wa Awasa ni moja ya viwanja vibovu katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati kutokana na kuwa na mabonde mabonde hivyo kufanya timu ngeni kuwa na kazi ya ziada kuzoea mazingira katika muda mfupi.
Lakini kwa upande wa mlinzi wa Simba na Taifa Stars, Victor Costa aliliambia gazeti hili kwa njia ya simu kuwa anaufahamu kwa undani uwanja huo hivyo Simba wasitarajie mteremko katika mchezo dhidi ya Awasa.
Timu ya Awasa ya nchini Ethiopia imepangwa kucheza na Simba katika michuano ya kombe la klabu bingwa Afrika mchezo utakaofanyika Februari mwaka huu, huku Yanga nayo ikiwa na kibarua kigumu cha kuwakilisha nchi katika michuanoa ya Kombe la Shirikisho.
Sunday, January 6, 2008
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment