Sunday, January 20, 2008

Dalali ampa somo Boban

Na Eunice Macha

Mwenyekiti wa Klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam, Hasan Dalali ametoa somo kwa mshambualiaji mahiri wa Timu ya hiyo na Taifa Stars, Haruna Moshi Boban kuwa mvumilivu wakati wa mechi za ligi kuu soka Tanzania Bara mzunguko wa pili ili kuepuka kufungiwa tena.


Akizungumza na Championi mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Dar es Salaam, Dalali alisema kwamba anamshauri Boban kuwa mvumilivu na maamuzi yanayotokea uwanjani ili kuepuka kukumbana na adhabu za TFF.

Aliongeza kuwa uwezo wa Boban ni mkubwa na kila mtu analijua hilo lakini kukosekana kwa uvumilivu kunaweza kusababisha kuidhoofisha timu kwani mchango wake ni muhimu kwa Simba na kwa taifa.

Aidha alifafanua kuwa maamuzi katika baadhi ya viwanja hapa nchini hayapendezi na yanakatisha tamaa kwa wachezaji lakini wanatakiwa kuwa wavumilivu kwa kutowapiga wala kuwatukana waamuzi kwani itasaidia kuondoa adhabu mbali mbali ikiwemo kufungiwa.

"Mimi Bobban nampenda sana kwa sababu anacheza kwa kujiamini, na stamina yake inamruhusu kucheza hata soka la Kimataifa ila tatizo lake ni hilo la kutokuelewana na baadhi ya waamuzi tu", alisema Dalali.

Haruna Moshi 'Boban' alifungiwa na kamati ya nidhamu ya shirikisho la soka nchini TFF muda wa miezi mitatu kwa kosa la utovu wa nidhamu hivyo kukosa baadhi ya mechi za mzunguko wa kwanza wa ligi kuu Tanzania Bara vile vile alikosa kucheza michuano ya CHALENJI ambapo Stars haikufika popote.

No comments: