




Na Ahadi Kakore
Serikali imesema kwamba klabu za Tanzania kufundishwa na makocha wa kigeni zaidi ya wazawa si suala geni bali jambo lillilozoeleka kwa miaka mingi katika soka la Tanzania.
Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo Seif Muhamed Khatib, ameiambia Championi kati kati ya wiki hii kwamba makocha wazalendo wanatakiwa kuacha kulalamikia hatua hiyo kwani suala hili lilikuwepo hata kabla ya kipindi hiki.
Khatib ambaye ni mshambuliaji wa zamani wa timu ya Caltex FC na timu ya Taifa ya Zanzibar, alisema kuwa makocha wazawa wanatakiwa kujiendeleza kielimu zaidi ili kulingana au kuwazidi hao wanaotoka nje.
Aliongeza kuwa suala la kucheza mpira si kigezo pekee cha kumfanya mtu kuwa kocha ila elimu na uwezo wa kufundisha ndivyo vitu vinayoweza kumfanya kocha kuwa bora.
"Suala la Timu za Taifa na klabu kufundishwa na Makocha kutoka nje si jambo la leo wala jana ila kinachotakiwa kwa makocha Wazalendo ni kujiendeleza zaidi kwa sababu wanaweza wakalalamika lakini wakawa hawana sifa kutokana na elimu zao kwa maana kila mtu duniani anahitaji kilicho bora," alisema Khatib.
Katika hatua nyingine Khatib alisema kwamba ari ya ushindani ya kutafuta makocha bora inayofanywa na klabu za Tanzania ni moja ya hatua ya maendeleo, ila wadau wa soka wanatakiwa kuwa wavumilivu kwani wengi wanataka mafanikio ya haraka kitu ambacho hakiwezekani kufanyika mara moja.
Klabu pekee nchini ambayo imejaza makocha wa kigeni ni Yanga ya jijini Dar es Salaam, ambapo hadi hivi sasa inamakocha wanne wa kutoka nje ya Tanzania ambao ni, Dusan Kondic, Spaso Sokolovsk, Zivojnov Srdan wote kutoka Serbia na Mmalawi Jack Chamangwana.
No comments:
Post a Comment