Thursday, March 20, 2008

Unyama!


Na Osoro Nyawangah, Magu

Hakika huu ni unyama wa aina yake ambao hauwezi kukunalika kwa mtu yeyote mwenye MOYO WA NYAMA labda kwa aliye na MOYO WA JIWE, hii imetokea ndani ya ardhi ya TANZANIA.

Mdau pata habari zaidi juu ya suala hili!!!!!

Mkazi mmoja wa Kitongoji cha Unyamwezini, Kijiji cha Itumbili, Kata ya Magu mjini wilayani Magu, Weja Mbula (31), amekimbilia Kituo Kikuu cha Polisi cha wilaya baada ya kumuua mkewe kwa kumkata kwa panga kichwani.

Kwa mujibu wa shuhuda ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, tukio hilo lilitokea hivi karibuni katika kijiji hicho baada ya mzozo

Habari zinasema kuwa, Mbula alianza kumshambulia mkewe, Kahabi Mwanzalima (28), kwa panga wakiwa ndani ya nyumba yao baada ya kuzuka kutokuelewana baina yao.

“Mbula alianza kumkata kwa panga kichwani mkewe na kuendelea kumshambulia hadi alipoanguka chini mita tano kutoka kwenye nyumba hiyo na kufariki papo hapo,” alisema mtoa habari huyo.

Mwandishi wetu ambaye alifika eneo la tukio muda mfupi baada ya mauaji hayo alifanikiwa na mpangaji mwenzao, aliyefahamika kwa jina la Yusta Machemla (61)

Machemla alisema kuwa wanandoa hao walianza kuzozana baada ya kutoka shambani ambako wanafanya kazi za kibarua kupanda mpunga.

“Kabla kifo cha mwanamke huyo, niliwasikia wakizozana kuhusu bei wanayotoza wateja wanaowalimia mashamba yao, ambapo marehemu alikuwa akimlalamikia mumewe kuwa anawatoza kiwango kidogo cha pesa kuliko kazi ngumu wanayoifanya,” alisema mtoa habari huyo

Aidha, Machemla aliongeza kuwa mwanamke huyo hakukubaliana na bei mumewe, hivyo kutaka awe (marehemu) akipatana bei na wateja wao.


Machemla ambaye wakati akiongea na mwandishi wetu nguo zake zilikuwa zimetapakaa damu, alisema kuwa mtuhumiwa huyo alimkata panga la kwanza kichwani wakati akitoka ndani ya nyumba kuchukua unga tayari kwa kusonga ugali.

“Baada ya hapo aliendelea kumkuta sehemu mbali mbali katika mwili wake hadi alipofariki,” alisema Machemla.


Mwenyekiti wa Kitongoji hicho, Charles Misungwi na Mwenyekiti wa Kijiji, Francis Ngh’onzela, wamweleza mwandishi wetu kuwa wananchi walimkamata mtuhumiwa ambaye alikuwa ameanza safari ya kujipeleka kituo cha polisi.


Kamanda wa Polisi Wilaya ya Magu(W), Philipo Kilangi, amethibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa na kusema kuwa jeshi limeanza kuchunguza tukio hilo.

“Mimi sio msemaji mwandishi lakini kama unavyoona suala hili liko wazi, tunamshikilia mtuhumiwa na taratibu za kipolisi zinaendelea”. alisema Kilangi.

WAZALENDO MEDIA TUNALAANI MAUAJI HAYA YA KUTISHA AMBAYO YANAWEZA KUBADILISHA MWELEKEO NA SURA YA WATANZANIA MBELE YA JUMUIYA YA KIMATAIFA, KWANI HILI NI JAMBO LISILOWEZA KUVUMILIWA NA YEYOTE.